NGUZA Mbangu,
mtoto mkubwa wa mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi anayetumikia
kifungo cha maisha jela, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya, amesema
mzazi wake pamoja na mdogo wake, Papii, ni lazima wataachiwa huru hivi
karibuni.
Mbangu, ambaye
pia hufahamika kisanii kama Mashine, ambaye hivi sasa ni mwinjilisti,
alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza na gazeti hili, akisema
kuwa kutolewa jela kwa ndugu zake hao, kutawafanya Watanzania kumsujudia
Mungu kupitia tukio hilo.
“Amini nakuambia, Mungu amenipa maono,
Babu Seya na Papii wako huru, watatoka tu, kinachosubiriwa ni muda tu
ambao hauko mbali, ni lazima watatoka kwa sababu hawana hatia,” alisema
Mbangu, ambaye pia alihukumiwa kifungo cha maisha jela kama mzazi wake,
lakini akaachiwa wakati walipokata rufaa kwa mara ya kwanza mahakamani.
Alisema
tukio hilo litakapotokea, litawafanya Watanzania wote kumsujudia
mwenyezi Mungu, kwa sababu litakuwa ni ishara ya uwezo wake katika
kutenda maajabu.
Babu Seya na Papii walihukumiwa kifungo cha maisha
jela mwaka 2004 baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi watoto wa
Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Sinza. Hata hivyo, jitihada zao za
kujinasua kwa mara ya mwisho ziligonga mwamba hivi karibuni baada ya
jopo la majaji watatu kutupilia mbali maombi ya kuachiliwa huru baada ya
kufanya mapitio ya kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi nchini.
No comments:
Post a Comment