

WAKATI
ikidaiwa kuwa majaliwa ya kiungo mshambuliaji Mrisho Ngassa kuwa
shakani kwenye klabu yake ya Azam, hali ya mambo sasa inaonyesha ni kama
filamu, kwani Ngassa ametamka wazi kuwa anaipenda klabu yake ya zamani
ya Yanga ambayo imekuwa ikihusishwa kumsajili.
Ngassa ambaye
aliifungia Azam bao la ushindi timu yake katika mechi ya nusu fainali
Kombe la Kagame dhidi ya Vita Club ya DR Congo, jana kwenye Uwanja wa
Taifa, aliwafuata mashabiki wa Yanga na kushangilia pamoja nao kisha
baada ya mechi akarejea tena jukwaani hapo na kupewa jezi ya Yanga kisha
kuivaa.
Ngassa aliyekuwa mchezaji pekee wa Azam akishangiliwa na
mashabiki wa Yanga katika mchezo huo, baada ya mechi hakutoka uwanjani
katika njia moja na wenzake badala yake alielekea kwenye lango
lililokuwa na mashabiki wa Yanga ambapo ndipo alipopewa jezi hiyo na
kuivaa.
Wakati huo wachezaji wenzake wa Azam FC tayari walikuwa
wamerejea vyumbani huku wakisherekea. Baadaye Ngassa aliungana nao akiwa
na jezi hiyo ya Yanga aliyoivaa juu ya jezi ya Azam.
“Naipenda Yanga
kwa kuwa nimetoka nayo mbali, natamani kurudi ila naheshimu mkataba
nilionao kwenye Azam, bao nililofunga limerejesha heshima yangu
iliyopotea muda mrefu, kuna mengi yanayoendelea lakini huu siyo muda
wake wa kuyazungumza,” alisema Ngassa.
Kumekuwa na taarifa kuwa
Ngassa hana uhusiano mzuri na kocha wake katika klabu ya Azam, Stewart
Hall na ndiyo maana amekuwa hampangi licha ya kuwa bado yupo kwenye
kiwango cha juu.
Alipoulizwa juu ya hilo Hall alisema: “Ngassa ni
mchezaji mzuri lakini anahitaji kujituma zaidi ili endelee kucheza
kwenye kikosi cha kwanza.”
Mara kadhaa, Ngassa amekuwa akionekana
makao makuu ya Yanga mitaa ya Jangwani na Twiga na ilielezwa ilichukua
miezi kadhaa kabla ya kurejesha funguo za chumba alichokuwa akikitumia
wakati akiwa Yanga.
Ngassa alijiunga na Azam FC kwa kitita cha Sh milioni 98 akitokea Yanga, hata hivyo ameshindwa kuonyesha cheche zake.
No comments:
Post a Comment