Kwa muda mrefu sana watangazaji mbalimbali wa redio za mikoani wamekuwa wakiniomba niwafikishie malalamiko yao kwa wasanii wa Tanzania. leo tu watangazaji wa kituo cha Kings FM ambao ni Robby Dabby na Jose M'bongo aka Teja wa muziki wamelizungumzia hili kupitia kipindi cha FIRE BEATZ.
Lisemwalo lipo na kama linasemwa na watangazaji wengi, basi si la kupuuza katu. Hii imekuwa inatokea sana kwa watangazaji wa redio hizo pale wanapotaka kufanya interview na wasanii, mara nyingi kwa simu. Wapo ambao huwachukulia kwa uzito na kuongea nao huku wakiwapa heshima ile ile ambayo wanaweza kumpa mtangazaji wa Clouds FM au East Africa Radio.
Mara nyingi baadhi ya wasanii huamini kuwa hizi redio za mikoani zinasikika katika eneo dogo na hivyo hata kama wakifanyiwa interview haiwezi kuwasaidia kwa lolote, haiendi popote. Hii sio kweli kwasababu redio za mikoani zina wasikilizaji wengi ambao ni mashabiki wa wasanii hawa pia mfano wa Redio Kings fm Ambayo inasikilizwa sana nje ya mkoa wa Njombe kupitia tune In hata ndugu Jonathan C.E.O wa huu mtandao huisifia na kuwa msikilizaji mzuri Online.
Redio za mikoani na wilayani zimekuwa zikifanya kazi kubwa kupromote kazi za wasanii, hivyo watangazaji wake wanahitaji kupewa uzito sawa kama ambavyo wasanii huwapa wale waliopo Dar es Salaam.
Wasanii wanapaswa kuwapa ushirikiano watangazaji hawa kwasababu kazi wanayofanya ni kuzicheza nyimbo zao na kuwaongezea mashabiki, wanapaswa kuwachukulia kama marafiki zao muhimu. Mashabiki wa wasanii hawa wana haki ya kuwasikia wasanii wanaowapenda wakihojiwa pia kwenye redio za maeneo yao.
Nafahamu kuwa redio kwa sasa zimekuwa nyingi na hivyo wasanii hujikuta wakipokea simu kibao za interview hadi kuwachosha kuongea na kuhitaji kupumzika. Huwachosha zaidi kwakuwa mara nyingi huulizwa maswali yale yale. Lakini watambue kuwa wao ni watu maarufu na kuhojiwa na waandishi na watangazaji ni sehemu muhimu katika career zao, hawawezi kukwepa. Wanapaswa kuwachukulia watangazaji wa redio zote kwa usawa.
No comments:
Post a Comment